Publisher's Synopsis
Kitabu hiki Mwenge wa Matumaini ni mwendelezo wa vitabu vya Christopher R. Mwashinga vilivyosheheni mashairi yaletayo matumaini na kumpatia msomaji kujiamini na ujasiri wa kukabili changamoto za Maisha. Mwandishi huyu anaamini kwamba njia mojawapo bora ya kupambana na hali ya ugumu au mambo yanayokatisha tamaa maishani, ni kuuinua mwenge wa matumaini kwa kuleta maneno mazuri yatiayo moyo na kurejesha matumaini. Kwa hivyo, maneno ya matumaini na kutia moyo yaliyomo katika tungo hizi mpya yamekusudiwa kugusa moyo wa msomaji na kumtia shime anapoendelea na safari yake ya maisha. Mashairi haya yatamsaidia msomaji kuzikabili siku za usoni kwa moyo wa ujasiri, matumaini na kujiamini zaidi huku akimtegemea Mungu aliye chanzo cha uhai wa kila mwanadamu.
Pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili wapenzi wa lugha ya Kiswahili duniani kwa ujumla siku za karibuni lugha ya Kiswahili imepata heshima ya kuketi viti vya mbele zaidi katika ulingo wa kimataifa. Mkutano Mkuu wa 41 wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, (UNESCO), Novemba 23, 2021 ulipitisha azimio namba 41C/61 la kutangaza tarehe 7 mwezi Julai kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani. Tangazo hilo limeleta furaha na kuongeza matumaini makubwa miongoni mwa wapenzi wa Kiswahili duniani. Kama sehemu ya kusherehekea mafanikio hayo ya lugha yetu adhimu ya Kiswahili, kitabu hiki kinakuletea mashairi mawili yenye ujumbe mahsusi wa kukienzi Kiswahili: "Kiswahili Kinapaa," na "Kiswahili Kilimbwende." Bila shaka kitabu hiki ni moja ya vitabu vya mwanzo kabisa vya ushairi ya Kiswahili kuchapishwa baada ya tangazo hilo muhimu kutolewa na Umoja wa Mataifa.
Ili kuchochea utamu wa ushairi na burudiko katika uzoefu wa msomaji, kitabu hiki kimesheheni mashairi yaliyoandikwa katika bahari tofauti tofauti ikiwa ni pamoja na mathnawi, ukawafi, mavue, ukaraguni, ukara, mtiririko, msuko, na utenzi. Vile vile, kwa mara nyingine mwandishi ameweka mashairi kadhaa yaliyoandikwa kwa mtindo wenye asili ya Kifaransa uitwao, Rondeau. Kwa Kiswahili bahari hii tunaiita bahari ya randuu. Ni matumaini yetu kwamba kitabu hiki kitawasha mwenge wa matumaini katika maisha ya msomaji popote pale alipo ulimwenguni.